Zimbabwe African National Liberation Army

Zimbabwe African National Liberation Army (ZANLA) ilikuwa mkono wa kijeshi wa chama cha Zimbabwe African National Union (ZANU) katika vita ya msituni ya Rhodesia iliyoleta uhuru wa Zimbabwe. Ilipigana na jeshi la Rhodesia Kusini pamoja na jeshi la ZIPRA ingawa pande zote mbili zilifuata itikadi tofauti na wakati mwingine kupigana kati yao.

ZANLA ilianzishwa mwaka 1965 huko Tanzania na hadi 1970 hivi makambi yake yalikuwa nje ya Rhodesia Kusini katika Zambia. Baadaye vikosi vyake vilikaa hasa Msumbiji.

Kiongozi wa kwanza wa ZANLA alikuwa Herbert Chitepo aliyefuatwa na Josiah Tongogara kuanzia 1973 hadi kifo chake 1979. Ilhali vita ilieleka kuisha Robert Mugabe alichukua uongozi aliyewahi kuongoza mkono wa kisiasa, yaani ZANU.

Mwanzoni ZANLA ililenga kushambulia jeshi la Rhodesia lakini kuanzia 1972 ilitumia mbinu za vita ya msituni kwa kufuata mfano wa wanamgambo wa Mao Tse Tung; mbinu hizi ziliwahi kutumiwa na jeshi la FRELIMO pale Msumbiji: kupeleka wanamgambo vijijini kwa siri, kufundisha wakulima na kutafuta wanamgambo wapya kati yao na kupanga mashambulio madogo.

ZANLA ilipata msaada kutoka China pamoja silaha na walimu wa kijeshi na kisiasa.[1]

Mugabe mwenyewe aliwahi kujitambulisha kuwa "Mfuasi wa Umarx-Ulenin upanda wa Mao" hivyo ZANLA na ZANU hawakupokea usaidizi kutoka Urusi iliyosaidia pekee jshi la ZIPRA.[2]

Itikadi ya ZANLA na ZANU ilipangwa kufuatana na mafundisho ya ukomomunisti wa Kichina kwa hiyo walijitazama kama kikosi cha mbele kitakachoongoza wananchi kuelekea mapinduzi. Ukosoaji ndani ya chama haukuvumiliwa.[3]: 6  Mwanahistoria wa Afrika Kusini, Sabelo Ndlovu-Gatsheni aliona ZANLA kuwa na muundo ambako takaso za kisiasa (ziliitwa kwa neno la Kishona "gukurahundi") ambako maafisa waliuawa zilitokea mra kwa mara na maafisa yake walitakiwa kutekeleza amri zozote bila kuonyesha mashaka.[3]: 6  Kiongozi mmoja wa ZANLA Edson Zvobgo alitaja kuwa "itikadi ya bunduki" ilikuwa suluhisho bora kwa kuondoa matatizo na maafisa wa ZANU wawe tayari kufyeka maadui wote wa chama.[3]: 12  Mauaji ya maafisa waliotofautiana na siasa rasmi ya uongozi yalitokea mara kwa mara.[3]: 12 

ZANLA ilishirikiana karibu na FRELIMO wa Msumbiji. Kuanzia 1972 makambi yake makuu yalikuwepo kwenye Mkoa wa Tete katika kaskazini ya Msumbiji. Baada ya uhuru wa Msumbiji 1975 ZANLA iliruhusiwa kutumia makambi kote kwenye mpaka baina ya Rhodesia na Msumbiji.

  1. Mutanda, Darlington (2017). The Rhodesian Air Force in Zimbabwe's war of liberation, 1966-1980. Jefferson, North Carolina: McFarland & Company, Inc., Publishers. uk. 177. ISBN 978-1476666204.
  2. Andrew, Christopher; Gordievsky, Oleg (1990). KGB : the inside story of its foreign operations from Lenin to Gorbachev. New York, NY: HarperCollinsPublishers. uk. 465. ISBN 9780060166052.
  3. 3.0 3.1 3.2 3.3 Ndlovu-Gatsheni, Sabelo J. (18 Oktoba 2013). "Rethinking Chimurenga and Gukurahundi in Zimbabwe: A Critique of Partisan National History". African Studies Review. 55 (03). doi:10.1017/S0002020600007186.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Tubidy